Biblia Habari Njema

Yohane 14:14-31 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.

15. “Mkinipenda mtazishika amri zangu.

16. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.

17. Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.

18. “Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu.

19. Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.

20. Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.

21. Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

22. Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”

23. Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.

24. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.

25. “Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi,

26. lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.

27. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.

28. Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.

29. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.

30. Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;

31. lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!