Biblia Habari Njema

Yohane 14:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.

11. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.

12. Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba.

13. Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.

14. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.

15. “Mkinipenda mtazishika amri zangu.

16. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.

17. Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.