Biblia Habari Njema

Yohane 13:19-28 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa ‘Mimi Ndimi.’

20. Kweli nawaambieni: Anayempokea yule ninayemtuma ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.”

21. Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!”

22. Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani.

23. Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.

24. Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.”

25. Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?”

26. Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.

27. Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!”

28. Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.