Biblia Habari Njema

Yohane 13:15-34 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.

16. Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu kuliko yule aliyemtuma.

17. Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.

18. “Haya nisemayo hayawahusu nyinyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: ‘Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.’

19. Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa ‘Mimi Ndimi.’

20. Kweli nawaambieni: Anayempokea yule ninayemtuma ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.”

21. Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!”

22. Wanafunzi wakatazamana wasiweze kabisa kujua anamsema nani.

23. Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.

24. Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: “Mwulize anasema juu ya nani.”

25. Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, “Bwana, ni nani?”

26. Yesu akajibu, “Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye.” Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.

27. Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, “Unachotaka kufanya, kifanye haraka!”

28. Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.

29. Kwa kuwa Yuda alikuwa mweka hazina, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.

30. Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.

31. Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.

32. Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara.

33. “Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: ‘Niendako nyinyi hamwezi kwenda!’

34. Nawapeni amri mpya: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi.