Biblia Habari Njema

Yohane 12:6-25 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.

7. Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.

8. Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.”

9. Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka kwa wafu.

10. Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro,

11. maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.

12. Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.

13. Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaza sauti wakisema:“Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.Abarikiwe mfalme wa Israeli.”

14. Yesu akampata mwanapunda mmoja, akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:

15. “Usiogope mji wa Siyoni!Tazama, Mfalme wako anakuja,amepanda mwanapunda!”

16. Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.

17. Kundi la watu wale waliokuwa pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka kwa wafu, walimshuhudia.

18. Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.

19. Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”

20. Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.

21. Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.”

22. Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.

23. Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!

24. Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.

25. Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele.