Biblia Habari Njema

Yohane 12:35-48 Biblia Habari Njema (BHN)

35. Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.

36. Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.

37. Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.

38. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia:“Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu?Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?”

39. Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena:

40. “Mungu ameyapofusha macho yao,amezipumbaza akili zao;wasione kwa macho yao,wasielewe kwa akili zao;wala wasinigeukie, asema Bwana,ili nipate kuwaponya.”

41. Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.

42. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi.

43. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu.

44. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.

45. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma.

46. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.

47. Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.

48. Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho.