Biblia Habari Njema

Yohane 11:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.

7. Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!”

8. Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?”

9. Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.

10. Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.”

11. Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.”

12. Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.”

13. Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.

14. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa;

15. lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.”

16. Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!”