Biblia Habari Njema

Yohane 11:36-48 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!”

37. Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?”

38. Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.

39. Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwisha anza kunuka; amekaa kaburini siku nne!”

40. Yesu akamwambia, “Je, sikukuambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?”

41. Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, “Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.

42. Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”

43. Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro! Toka nje!”

44. Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mkamwache aende zake.”

45. Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu, wakamwamini.

46. Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.

47. Kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza Kuu, wakasema, “Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno.

48. Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu hekalu letu na taifa letu!”