Biblia Habari Njema

Yohane 10:31-42 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.

32. Yesu akawaambia, “Nimewaonesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?”

33. Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya kazi njema, ila kwa sababu ya kumkufuru Mungu! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.”

34. Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika sheria yenu: ‘Mimi nimesema, nyinyi ni miungu?’

35. Mungu aliwaita miungu wale waliopewa ujumbe wake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.

36. Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: ‘Unakufuru,’ eti kwa sababu nilisema: ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’

37. Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini.

38. Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi, mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake.”

39. Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.

40. Yesu akaenda tena ngambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.

41. Watu wengi walimwendea wakasema, “Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa.”

42. Watu wengi mahali hapo wakamwamini.