Biblia Habari Njema

Yohane 10:23-35 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Naye Yesu akawa anatembea hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.

24. Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, “Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiwe Kristo, basi, tuambie wazi.”

25. Yesu akawajibu, “Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.

26. Lakini nyinyi hamsadiki kwa sababu nyinyi si kondoo wangu.

27. Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.

28. Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.

29. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.

30. Mimi na Baba, tu mmoja.”

31. Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.

32. Yesu akawaambia, “Nimewaonesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?”

33. Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya kazi njema, ila kwa sababu ya kumkufuru Mungu! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.”

34. Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika sheria yenu: ‘Mimi nimesema, nyinyi ni miungu?’

35. Mungu aliwaita miungu wale waliopewa ujumbe wake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.