Biblia Habari Njema

Yohane 1:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”

23. Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake:‘Sauti ya mtu anaita jangwani:Nyosheni njia ya Bwana.’”

24. Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.

25. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?”

26. Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.

27. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”

28. Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.

29. Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!

30. Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’

31. Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”

32. Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.

33. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’

34. Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”