Biblia Habari Njema

Yohane 1:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.

19. Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?”

20. Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”

21. Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”

22. Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”

23. Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake:‘Sauti ya mtu anaita jangwani:Nyosheni njia ya Bwana.’”

24. Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.

25. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?”

26. Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.

27. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”

28. Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.

29. Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!