Biblia Habari Njema

Yohane 1:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’”

16. Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema.

17. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo.

18. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.

19. Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?”

20. Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”

21. Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”

22. Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”

23. Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake:‘Sauti ya mtu anaita jangwani:Nyosheni njia ya Bwana.’”