Biblia Habari Njema

Mhubiri 8:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Naam, kila kitu kina wakati wake na njia yake, ingawa binadamu anakabiliwa na tatizo kubwa:

7. Hajui ni nini kitakachotukia baadaye, kwani nani awezaye kumjulisha yatakayotukia baadaye?

8. Hakuna mtu aliye na uwezo wa kushikilia roho yake asife; hakuna mtu aliye na uwezo juu ya siku ya kufa. Wakati wa vita hakuna kuponyoka, na uovu hauwezi kumwokoa mwovu.

9. Haya yote nimeyaona katika uchunguzi wangu juu ya yote yanayotendwa hapa duniani, binadamu anapokuwa na uwezo wa kumkandamiza na kumdhuru binadamu mwenzake.

10. Tena, nimewaona waovu wakizikwa, na watu waliporudi kutoka mahali patakatifu wanawasifu humohumo mjini walimotenda maovu yao. Hayo nayo ni bure kabisa.

11. Kwa vile uovu haupatilizwi haraka, mioyo ya wanadamu hupania kutenda mabaya.

12. Wenye dhambi hutenda maovu mara mia, hata hivyo, huendelea kuishi. Walakini, mimi najua kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, kwa sababu ya uchaji wao;