Biblia Habari Njema

Matendo 7:31-41 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:

32. ‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.

33. Bwana akamwambia: ‘Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu.

34. Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.’

35. “Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?’ Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.

36. Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani, kwa muda wa miaka arubaini.

37. Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: ‘Mungu atawateulieni nabii kama mimi miongoni mwa ndugu zenu nyinyi wenyewe.’

38. Waisraeli walipokusanyika kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko kama mjumbe kati ya hao wazee wetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai. Ndiye aliyekabidhiwa yale maneno ya uhai atupe sisi.

39. “Lakini yeye ndiye babu zetu waliyekataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.

40. Walimwambia Aroni: ‘Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata huyo Mose aliyetuongoza kutoka Misri!’

41. Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.