Biblia Habari Njema

Matendo 21:28-40 Biblia Habari Njema (BHN)

28. wakipiga kelele: “Wananchi wa Israeli, msaada, msaada! Huyu ndiye yule mtu anayewafundisha watu kila mahali mambo yanayopinga watu wa Israeli, yanayopinga sheria ya Mose na mahali hapa patakatifu. Hata sasa amewaingiza watu wa mataifa mengine hekaluni na kupatia unajisi mahali hapa patakatifu.”

29. Sababu ya kusema hivyo ni kwamba walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa pamoja na Paulo mjini, wakadhani kwamba Paulo alikuwa amemwingiza hekaluni.

30. Mji wote ulienea ghasia; watu wakaja kutoka pande zote, wakamkamata Paulo, wakamburuta, wakamtoa nje ya hekalu, na papo hapo milango ya hekalu ikafungwa.

31. Walikuwa tayari kumwua, lakini habari zilimfikia mkuu wa jeshi la Kiroma kuwa Yerusalemu yote ilikuwa imejaa ghasia.

32. Mara, mkuu wa jeshi akawachukua askari na jemadari, akalikabili lile kundi la watu. Nao walipomwona mkuu wa jeshi na askari, wakaacha kumpiga Paulo.

33. Mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamtia nguvuni na kuamuru afungwe minyororo miwili. Kisha akauliza, “Ni mtu gani huyu, na amefanya nini?”

34. Wengine katika lile kundi la watu walikuwa wanapayuka kitu hiki na wengine kitu kingine. Kwa sababu ya ghasia hiyo, mkuu wa jeshi hakufaulu kujua kisa kamili. Hivyo, aliamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome.

35. Paulo alipofika kwenye ngazi, askari walilazimika kumbeba kwa sababu ya fujo za watu.

36. Kwa maana watu kundi kubwa walimfuata wakipiga kelele, “Mwulie mbali!”

37. Walipokuwa wanamwingiza ndani ya ngome, Paulo alimwomba mkuu wa jeshi akisema, “Naweza kukuambia kitu?” Yule mkuu wa jeshi akamjibu, “Je, unajua Kigiriki?

38. Kwani wewe si yule Mmisri ambaye hivi majuzi alianzisha uasi na kuwaongoza majahili 4,000 hadi jangwani?”

39. Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia; mimi ni raia wa mji maarufu. Tafadhali, niruhusu niongee na watu.”

40. Yule mkuu wa jeshi akamruhusu. Hivyo Paulo alisimama juu ya ngazi, akawapungia mkono wale watu, na walipokaa kimya, akaanza kuongea nao kwa Kiebrania: