Biblia Habari Njema

Matendo 2:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.

5. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.

6. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?

8. Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?

9. Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,

10. Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,

11. Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.”