Biblia Habari Njema

Matendo 17:6-14 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini.

7. Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti: ‘Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.’”

8. Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu.

9. Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.

10. Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.

11. Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli.

12. Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.

13. Lakini, Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.

14. Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea.