Biblia Habari Njema

Luka 9:46-56 Biblia Habari Njema (BHN)

46. Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi.

47. Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye,

48. akawaambia, “Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

49. Yohane alidakia na kusema, “Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.”

50. Lakini Yesu akamwambia, “Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu.”

51. Wakati ulipokaribia ambapo Yesu angechukuliwa juu mbinguni, yeye alikata shauri kwenda Yerusalemu.

52. Basi, akawatuma wajumbe wamtangulie, nao wakaenda wakaingia kijiji kimoja cha Wasamaria ili wamtayarishie mahali.

53. Lakini wenyeji wa hapo hawakutaka kumpokea kwa sababu alikuwa anaelekea Yerusalemu.

54. Basi, wanafunzi wake, kina Yohane na Yakobo, walipoona hayo, wakasema, “Bwana, wataka tuamuru moto ushuke kutoka mbinguni uwateketeze?”

55. Lakini yeye akawageukia, akawakemea.

56. Wakatoka, wakaenda kijiji kingine.