Biblia Habari Njema

Luka 24:30-41 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.

31. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.

32. Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?”

33. Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika

34. wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.”

35. Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.

36. Walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani iwe nanyi.”

37. Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.

38. Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu?

39. Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkaone, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.”

40. Baada ya kusema hayo, akawaonesha mikono na miguu.

41. Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?”