Biblia Habari Njema

Luka 19:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, kabla ya kuondoka, aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kuwaambia: ‘Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.’

14. Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: ‘Hatumtaki huyu atutawale.’

15. “Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.

16. Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.’

17. Naye akamwambia: ‘Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!’

18. Mtumishi wa pili akaja, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.’

19. Naye akamwambia pia: ‘Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.’

20. “Mtumishi mwingine akaja, akasema: ‘Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,

21. kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na kuchuma ambacho hukupanda.’

22. Naye akamwambia: ‘Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.

23. Kwa nini, basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?’