Biblia Habari Njema

Luka 12:51-59 Biblia Habari Njema (BHN)

51. Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano.

52. Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.

53. Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mamamkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mamamkwe wake.”

54. Yesu akayaambia tena makundi ya watu, “Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: ‘Mvua itanyesha,’ na kweli hunyesha.

55. Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema ‘Kutakuwa na joto,’ na ndivyo inavyokuwa.

56. Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia hali ya nchi na anga; kwa nini, basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?

57. “Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya?

58. Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani.

59. Hakika hutatoka huko, nakuambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho.”