Biblia Habari Njema

2 Wafalme 25:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale wote waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na watu wengine wote.

12. Lakini aliacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini. Aliwaacha watunze mizabibu na kulima mashamba.

13. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, pamoja na vikalio vyake, birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi mpaka Babuloni.

14. Vilevile walichukua vyungu, masepetu, makasi na miiko iliyotumiwa kuchomea ubani na vyombo vingine vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu,

15. wakachukua na vyetezo na mabakuli. Kapteni wa walinzi wa mfalme alipeleka mbali kila chombo cha dhahabu na kila chombo cha fedha.

16. Shaba yote nyeusi aliyotumia Solomoni kutengeneza zile nguzo mbili, birika lile kubwa na vikalio kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu haikuweza kupimwa kwa uzito.

17. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa mita 8, na juu yake kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi, urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 1.25. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi.

18. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, Sefania kuhani wa pili pamoja na maofisa walinda milango watatu;