Biblia Habari Njema

2 Wafalme 24:12-20 Biblia Habari Njema (BHN)

12. na Yehoyakini mfalme wa Yuda alijisalimisha kwa mfalme wa Babuloni, yeye mwenyewe pamoja na mama yake, watumishi wake, maofisa na maakida wake. Mfalme wa Babuloni alimchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.

13. Vilevile, pia kama Mwenyezi-Mungu alivyosema, Nebukadneza alichukua mali yote iliyokuwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ndani ya ikulu. Alikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alitengeneza. Vyombo hivyo vilikuwa ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu.

14. Alichukua watu wote wa Yerusalemu: Wakuu wote, watu wote waliokuwa mashujaa, mateka 10,000, na mafundi wote na wahunzi. Hakuna aliyebaki isipokuwa waliokuwa maskini kabisa nchini.

15. Alimchukua Yehoyakini mpaka Babuloni pamoja na mama yake mfalme, wake za mfalme, maofisa wake na wakuu wa nchi; wote hao aliwatoa Yerusalemu, akawapeleka Babuloni.

16. Nebukadneza alichukua watu mashujaa wa Yuda jumla yao watu 7,000 pamoja na mafundi hodari na wahunzi 1,000; wote hawa wakiwa watu wenye nguvu na wa kuweza kupigana vitani.

17. Nebukadneza akamtawaza Matania, mjomba wake Yehoyakini, kuwa mfalme badala yake, akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.

18. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Libna.

19. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile alivyofanya mfalme Yehoyakimu.

20. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda, hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni.