Biblia Habari Njema

2 Wafalme 20:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huo Hezekia aliugua sana karibu na kufa. Ndipo nabii Isaya, mwana wa Amozi alipomwendea na kumwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu; ‘Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.’”

2. Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu akisema,

3. “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.

4. Lakini kabla Isaya hajapita ua wa katikati, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia, kusema,

5. “Rudi ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wa Mwenyezi-Mungu: Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu yako Daudi, nimesikia ombi lako na nimeona machozi yako. Nitakuponya na baada ya siku tatu utakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

6. Nitakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi.”

7. Basi Isaya akasema, “Leteni andazi la tini mliweke kwenye jipu lake, ili apate kupona.”

8. Hezekia akamwuliza Isaya, “Ni ishara gani ambayo itanionesha kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ataniponya na katika siku ya tatu nitaweza kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?”

9. Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele au nyuma?”

10. Hezekia akamjibu, “Ni rahisi zaidi kivuli kwenda mbele hatua kumi! Hebu kirudi nyuma hatua kumi.”