Biblia Habari Njema

1 Wafalme 22:26-35 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya; mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme.

27. Waambie wamtie gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.”

28. Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama basi, utajua kwamba Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikilizeni enyi watu wote!”

29. Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na mfalme Yehoshafati wa Yuda, kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi.

30. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme na kuingia vitani lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme.

31. Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake thelathini na wawili waliosimamia magari yake ya kukokotwa, akisema: “Msipigane na mtu yeyote yule, mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.”

32. Baadaye, makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema: “Kweli, huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea, wakamshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele.

33. Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli waliacha kumshambulia, wakarudi.

34. Lakini, askari mmoja wa Aramu, akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma kifuani. Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Geuza gari uniondoe vitani. Nimejeruhiwa!”

35. Na mapigano siku hiyo yakazidi kuwa makali, huku mfalme ameegemeshwa garini, anawaelekea watu wa Aramu. Ilipofika jioni, akafariki. Damu ikawa inamtoka jerahani mwake na kutiririka hadi chini ya gari.